Muonekano
Lugha
Somo yake Bi Neema ndiye aliyemsababishia janga ambalo hatalisahau mpaka aendapo kuzimu. Laiti angefuata ushauri wa Dokta Faiz au hata angesikiliza onyo la shoga yake, Selina! Huenda angejiepusha na janga hilo. Wala asingekuwa na sababu ya kumlalamikia kila mtu kwamba “SOMO KANIPONZA”
Kwa njia moja au nyengine, karatasi hizo LAZIMA zipatikane… LUTENI JOSHUA anatoroka na karatasi za siri alizozipata nyumbani kwa Iddi Amin mara tu Nduli huyo alipoikimbia Uganda. Karatasi hizo zinatakiwa na nchi kadhaa za Afrika. Ray Sibanda, mpelelezi wa Tanzania anapelekwa Nairobi ambako ndiko aliko Luteni Joshua ili akazitafute karatasi hizo na amrejeshe Luteni huyo nyumbani. Lakini si Tanzania peke yake inayopeleka mpelelezi wake Nairobi. Uganda na Libya pia wamo mbioni. Msumbuji inapeleka mpelelezi wake wa kike, Ida Ymana, ambaye ni hatari zaidi kuliko hizo karatasi zenyewe. Mkusanyiko wa wapelelezi hao wanne mjini Nairobi unaifanya kazi ya kuzisaka karatasi hizo iwe ya ROHO MKONONI.
Niliwaonya lakini hawakusikia, hatimaye uvumilivu ukanishinda. Na sasa ni Ama Zao Ama Zangu.
Riwaya hii, SANDA YA JAMBAZI, inaendeleza pale ilipoishia ile riwaya iliyowasisimua wengi, UKIMWONA MMALIZE! Inspekta Sindi na Koplo Fideli, ambae hivi karibuni amepandishwa cheo na kuwa Sajenti, ndio waliokuwa wakishughulikia upelelezi katika riwaya hiyo na kukutana nao tena katika riwaya hii. Jambazi linalohusika ni lile lile Malik Mbowe. Katika kulifukuza jambazi hilo, Inspekta Sindi na Koplo Fideli walikaribia kulinasa; lakini jitu kama Malik Mbowe halinasiki kirahisi. Sindi alimtaka Malik aweke bastola yake chini na anyooshe mikono juu. Kwamba jambazi hilo lilifikia mwisho wake. Malik alimpuuza. “Hunipati kirahisi, Sindi,” alimwambia, papo hapo akafyatua risasi mbili, akaunyakua mkoba wake. Alipoanza kutimua mbio, Inspekta Sindi aliinua bastola yake akafyatua risasi moja tu. Wote wawili, Inspekta Sindi na Koplo Fideli, walimwona akiangukia bondeni huku mkono wake ukishikilia bega lililojeruhiwa vibaya. Alipiga kelele nyingi za maumivu. Hawakumwona tena! Ni baada ya askari hao wawili kufika nyumbani kwa Perino na kushuhudia yaliyotokea ndipo Sindi alipoamua yasambazwe matangazo nchini nzima na picha yake, kwamba yeyote atakayemwona jambazi huyo, popote pale, ammalize japokuwa alikuwa na uhakika kuwa Malik asingeweza kutoka mle bondeni hai. Alikosea sana! Malik alikuwa na roho ngumu kama ya paka. Japo alijeruhiwa vibaya lakini alipona. Na balaa alilozusha huko alikokwenda halisemeki! Sasa endelea…
Baada ya kuagana na mumewe kwa masikitiko, Diana Msangi anaapa kutoshiriki katika jambo lolote la starehe hadi hapo mumewe Mathias Kamara atakaporejea kutoka Mwanza. Maskini Diana hakutambua kuwa rafiki yake Lucy angeweza kumlaghai na kumtumbukiza katika janga lisilo na kina….
“We chekelea tu hiyo safari ya Dar.” Shangazi alinionya huku akibetua mdomo. “Humalizi hata miezi mitatu utarudi kitumbo ndii huku umenuna.” Kwani nilimjibu? Niliona ananionea gere. Nikaondoka. Sikumaliza hata mwezi, balaa likaanza. Shemeji yangu, mume wa dada’angu baba mmoja, mama mmoja. Aliniingilia chumbani usiku akataka kuni… aah si unajua tena? Na ningemchekea angenivimbisha kweli tumbo! Ndipo nilipomkatalia katakata: SITAKI- Sijavunja Ungo!
“Kwa mume kuna ngondo Mwanahamisi hakuna uhondo. Wala hakuna utamu kuna balagham! Ndivyo alivyonamboa somo yangu Mama Muhidini kabla sijaolewa. Nilidhani anatania. Loh! Nyumba niliiyona kama kaburi babu, GUBU LA MUME lilinishinda.
Waswahili husema, kila mchuma janga hula na wakwao. Lakini msemo huu kwa Issa umekuwa ni tofauti baada ya kukosa mtu wa kula nae janga alilolichuma. Laiti kama asingeonywa au kuambiwa acha! Angekuwa na kila sababu ya kulalama. Ila ndiyo hivyo, sikio la kufa siku zote halisikii dawa, alifanya alichoona ni sahihi kwake. Sasa anahaha baada ya maji kumfika shingoni. Kwani ana la kusema? Si AMEJITAKIA mwenyewe!
Kigenda Bakari, mke wa Akida. Mwanamke anayeamua kujifunga kibwebwe kuipambania ndoa yake baada ya kuchoshwa na visa na vioja vya mkwewe. Mkwewe, Bi. Mwanamtoo, alishajipanga. Visa, chuki, visirani, gubu na usihiri anavitumia kama silaha ya kujimilikisha nyumba anayolipa kodi mwanawe wa kumzaa. “Lakini ni mume wangu.” “Na mimi ni mama yake.” Zogo linapovuka mipaka na kuwa shonde, nyumba nayo inageuka kuwa uwanja wa mapambano. Je, Kigenda ataliweza shonde la mama mkwe?
Kwa jina la baba ni moja kazi yenye viwango kutoka kwa Mwandishi nguli nchini Tanzania Crarency Sanga. Ukianza kuisoma hutaiacha.
Mwandishi Crarency Sanga ni mzuri katika usimuliaji wa simulizi za maisha ya kawaida, lakini pia ni mzuri zaidi katika simimulizi za kijasusi, mapigano na upelelezi. Hapa unakutana naye katika kitabu cha The Red Congo, hakika ukianza kukisoma utasahau kufanya shughuli nyingine.
Upo wakati moyo wa mtu hutamani visivyotamanika. Hapa kwa dhati unaaswa kuepuka sana kuangukia mtegoni kwa sababu ya moyo wako na kuamua kuziacha akili zako bila faida. Kitakukuta kikubwa cha kutamausha! Katika riwaya hii, japo si mara zote, Panga, kijana mtanashati, muungwana wa mtaa, anajikuta akiingia katikati ya dimbwi refu la mapenzi, lililojawa tope la kila hiana na laana, anashikika barabara hata mishipa yake ya fahamu inapumbaa. Hajitambui! Nduguze walimkanya na kumjuza juu ya uraibu hatari wa huba, kuwa alipitiwa na kuiacha njia, hakusikia. Moyowe ushapenda na kufa, unadhani sikio litakuwa na nafasi ya kuushawishi moyo? Fuatilia kisa hiki cha kusisimua, “KirangaKomo” kilichojaa ucheshi, huzuni na misukosuko ya kuutikisa moyo na nafsi kutoka kwa mwandishi mwenye haiba iliyojengeka katika muktadha wa uswahilini waliko watu na mambo yao...ndiye Mtajika wa visa na mikasa hai.. Muddyb Mwanaharakati
Maisha ya walimwengu yamejaa visa na mikasa ya kusisimua. Hata hivyo, katika miji na majiji wanawake na wanaume huishi kila mmoja na mtindo wake ili kukidhi mahitaji ya kila siku. Katika harakati za kuisaka riziki na kuiepa dhiki, hapa ndipo kudra na juhudi hujitokeza. Wapo wapatao mali na kuwa na maisha ya kustarehe na wapo ambao huishi kwa kuunga tumaini wakitegemea wenye nazo. Hapo ndipo kunazaliwa riwaya hii ya kusisimua, wahuni wote peponi. Tunakutana na Mwamba Mzeta na wahuni wenzake dhidi ya mdangaji aliyekubuhu, Sijali na mashogaze, akiwajumuisha Avijawa na Amina, hawa ni wenye kiu ya kuishi kwa jasho la waume ambao nao wanahitaji starehe ya faragha. Inakuwa kukomoana na kukomeshana. Japo mwandishi ameandika riwaya hii kwa wingi wa visa vya kuchekesha na lugha iliyojaa kejeli kutoka kwa wahusika, riwaya hii imeyaakisi maisha halisi ya wakazi wa jiji la Dar es salaam hasa TANDIKA, eneo la BUZA na maeneo mbalimbali ya jirani. Kutano la wahuni na wasaka riziki linazaa misukosuko ya maisha yanayopelekea vyombo vya dola kuwajibika kwa upande mmoja, lakini mwisho wa dhiki ni faraja. Kitabu hiki kitakufurahisha na kukufunza juu ya maisha ambayo hujawahi kuyawaza, kwani mengi hufanyika sirini lakini mwandishi amefanikiwa kuyaonesha kwa uwazi. Mwamba Mzeta ndiye aliyeasisi jina la kitabu hiki akiwa na wahuni wenzake kilingeni kwa kusema, “Wahuni wote peponi! Hatunaga unafiki— hiyo pekee inatuhusu!?